Hafla ya kuiaga Serengeti Girls, Mhe. Mchengerwa atoa maagizo mazito kwa Mkurugenzi mpya wa Michezo
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Septemba 21, 2022 amewaongoza watanzania kuiaga timu ya Serengeti Girls kwenda Kombe la Dunia huku akitoa maelekezo mahususi kwa Kaimu Mkurugenzi mpya wa Michezo kuhusu kuendeleza sekta hiyo.
Katika hafla ya kuiaga timu hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mhe. Mchengerwa amekabidhi BIMA na vifaa mbalimbali vya michezo ambapo pia Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi na wadau mbalimbali wa michezo walishiriki.
Mhe. Mchengerwa amemtaka Kaimu Mkurugenzi mpya, Ally Mayay kuleta maboresho kusudiwa kwenye Sekta ya Michezo na endapo hataweza ataondolewa.
Mbali na hayo, Mhe. Mchengerwa amempa maelekezo mahususi ambayo ametaka yafanyiwe kazi mara moja.
Maelekezo hayo ni pamoja na kuweka mfumo wa Kutafuta vipaji vya wachezaji Kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa ( BMT) na Shirikisho la Soka nchini (TFF) pia kuandaa mifumo ya kuwasajili wanamichezo kuanzia ngazi za Umitashumta na Umiseta na kuendelea kuwalea.
Ashirikiane na Wizara wadau wa michezo, kama TAMISEMI, Elimu ili kuja na mpango wa kuifanya michezo kuwa sehemu ya masomo ya nayofundishwa mashuleni.
Maelekezo mengine nikuboresha miundombinu ya michezo ikiwa ni pamoja na kukarabati viwanja vitano vya Soka ambavyo Serikali inakusudia kufanya ukarabati ili Tanzania iweze kufuzu kuratibu mashindano ya AFCON mwaka 2027.
Amesema dhamira ya Serikali na ndoto za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona kuwa Tanzania inaratibu mashindano hayo na hatimaye kombe la dunia.
Pia amemtaka aandae mara moja kanzidata ya walimu na wakufunzi wa michezo
Aidha, amemtaka kushirikisha wadau hususan balozi ambazo zipo tayari na mipango kazi ya kusaidia kujenga miundombinu ya michezo nchini.
Kwa upande wake, Ally Mayay amemshukuru Mhe. Waziri Mchengerwa kwa kumteua na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa.





 
 
 
Comments
Post a Comment