Waziri Mchengerwa aelekeza vilabu vyote kumiliki viwanja vyake vyenyewe, Yanga na Simba vyaahidi kutekeleza agizo hilo ndani ya miezi sita.
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Agosti 17, 2022 ameelekeza vilabu vyote kumiliki viwanja vyake vyenyewe ambapo timu ya Yanga na Simba zimeahidi kutekeleza agizo hilo ndani ya miezi sita.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo alipokutana na watendaji wakuu wa vilabu vinavyoshiriki ligi kuu jijini Dar es Salaam na kujadili namna bora ya kuendesha ligi kwa ubunifu na ushindani wa hali ya juu ili kuifanya ligi iwe na mvuto.
Mhe. Mchengerwa amesema mpango wa vilabu kumiliki viwanja vyao ni takwa la kisheri kulingana na Sera ya Michezo nchini.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa pamoja na mambo mengine kikao hicho kimejadili masuala ya kuzingatia weledi, nidhamu na maadili.
Amesema kwa sasa Serikali haiwezi kukubaliana na vitendo vyovyote vya rushwa na upendeleo katika michezo kwa kuwa vinasaidia kuua na kudidimiza michezo.
Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuendesha michezo kisasa ili kuleta maboresho makubwa yatakayosaidia kuifikisha Tanzania kwenye ramani ya kimataifa.
Viongozi hao wamemshukuru Waziri Mchengerwa kwa kuja na mpango huo wa kuwashirikisha viongozi ili waweze kujadili changamoto zao na Serikali na kupata ufumbuzi wa pamoja na wa kudumu.






 
 
 
Comments
Post a Comment