Mhe. Mchengerwa ahesabiwa, asisitiza watu wote kuhesabiwa
Na John Mapepele, Rufiji .
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa wanamichezo na wasanii wote kujitokeza kuhesabiwa ili Serikali iweze kupanga mipango ya maendeleo.
Akiongea mara baada ya kuhesabiwa leo, Agosti 23, 2022 kwenye makazi yake Ikwiriri - Rufiji amesema mafanikio ya kizazi cha kesho yatatokana na kujua idadi sahihi ya takwimu za sasa.
"Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa zoezi hili la sensa kwa kuwa linalokwenda kutusaidia sana kuleta maendeleo" ameingeza Mhe. Mchengerwa
Aidha, amesema sensa ya mwaka huu ni muhimu katika sekta za michezo, na sanaa kwa kuwa itasaidia kupanga namna bora ya kuwahudumia watanzania kwenye sekta hizo.
Amesema hiyo itasaidia kupanga namna na kujenga miundombinu ya michezo kama vile viwanja vya michezo na arena za michezo.
Amefafanua kuwa sensa itasaidia mipango ya kibajeti kuandaa kanzi data ya michezo na kutafuta vipaji vya wasanii na michezo.
Amesema kutokana na umuhimu wa zoezi hili Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliamua kuja na kampeni maalum ya SENSABIKA ya kuhamasisha watu wote kuhesabiwa.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa jimbo la Rufiji na watanzania wote kujitokeza kuhesabiwa.



Comments
Post a Comment